Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pande kinzani Sahara Magharibi acheni mvutano- Guterres

Pande kinzani Sahara Magharibi acheni mvutano- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuendelea kwa mvutano kwenye ukanda unaotenganisha pande kinzani huko Sahara Magharibi.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemnukuu Bwana Guterres akieleza kuwa mvutano huo ni kati ya vikosi vya Morocco na vile vya kiundi cha Polisario ambavyo vimekaribiana tangu mwezi Agosti mwaka jana na kuleta wasiwasi mkubwa.

Pande mbili hizo zimekuwa zinafuatiliwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa huko Sahara Magharibi, MINURSO.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa pande hizo kujizuia kuchukua hatua yoyote iwe ya kijeshi au kupitia raia, hatua ambazo amesema zinaweza kuongeza mvutano.

Amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha magari binafsi yanayopita eneo hilo hayazuiwi na kwamba isichukuliwe hatua yoyote ya kubadili hali iliyokubaliwa kuwepo kwenye ukanda huo usio na mapigano.

Badala yake ametaka pande hizo kuondoa vikosi vyao  hara iwezekanavyo na kuweka mazingira bora ya kurejesha mazungumzo kwa minajili ya mchakato wa kisiasa, mpango unaoongozwa na Umoja wa Mataifa.