Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yachapisha orodha ya bakteria sugu

WHO yachapisha orodha ya bakteria sugu

Shirika la afya ulimwenguni WHO, leo limechapisha orodha ya kwanza kabisa ya aina 12 za bakteria ambao ni tishio zaidi kwa afya ya binadamu. Joseph Msami na ripoti kamili.

(Taarifa ya Joseph Msami)

Taarifa ya WHO imesema kuwa orodha hiyo iliandaliwa kwa ajili ya kuongoza na kupigia chepuo utafiti na maendeleo ya viuavijasumu , ikiwa ni sehemu ya juhudi za shiriki hilo za kukabiliana na vidubini.

Mkurugenzi msaidizi wa WHO kuhusu mifumo ya afya na ubunifu, Dkt. Marie-Paul Kieny amesema orodha hiyo imegawanywa katika vipaumbele vitatu vya tafiti za haraka zaidi, haraka na kipaumbele cha kati ili dawa sahihi zipatikane kwa afya ya umma.

Mathalani amesema wanaohitaji uharaka zaidi ni bakteria tishio hospitali, makazi ya huduma ya afya na kwa wagonjwa ambao tiba zao hutegemea vifaa kama vile vya usaidizi wa kupumua.

Amesema bakteria wa kiwango hicho wamebaini njia ya kujibadili na hivyo kuwa sugu kwa dawa tofauti.

Hata hivyo amesema jawabu la kudumu si tafiti pekee bali kusaka njia mpya za kuzuia magonjwa, sambamba na matumizi sahihi ya viuavijasumu vilivyopo na vipya vitakavyogunduliwa.