Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumesikitishwa na hukumu ndogo kwa askari wa Israel aliyeua:UM

Tumesikitishwa na hukumu ndogo kwa askari wa Israel aliyeua:UM

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema imesikitishwa na hukumu ndogo iliyotolewa na mahakama ya kijeshi ya Tel Aviv mapema wiki hii dhidi ya askari wa Israel aliyekutwa na hatia ya mauaji ya raia wa Palestina aliyekuwa amejeruhiwa, kwa kile kinachojulikana kama amauaji ya kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya mtu aliyekuwa hana silaha na hakuwa tishio.

Sajenti Elor Azaria alikuwa na hatia ya mauaji ya bila kukusudia mwezi Januari mwaka huu kwa kumpiga risasi na muua Abdelfattah al-Sharif kwenye mji wa Hebron mwezi Machi mwaka 2016. Ravina Shamdasani ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu

(SAUTI YA RAVINA)

“Bwana Al-Sharif hakuwa na silaha yoyote na alikuwa amelala chini akiwa amejeruhiwa baada ya kupigwa risasi alipomchoma kisu na kumjeruhi askari wa Israel. Ingawa kosa la kuua bila kukusudia lina adhabu ya juu ya miaka 20 jela , sajenti Azaria alihukumiwa kwenda jela miezi 18 tu na kushushwa cheo”

Ofisi ya haki za binadamu inasema zaidi ya Wapalestina 200 wameuawa na wanajeshi wa Israel tangu kuzuka machafuko ya karibuni kwenye ukingo wa Magharibi mwaka 2015, na sajenti Azaria ndio askari pekee wa jeshi la Israel aliyeshitakiwa na kuhukumiwa kwa ajili ya mauaji hayo.

Ofisi hiyo imeongeza kwamba kesi hii inahatarisha uaminifu katika mfumo wa sheria na haki na kushamirisha utamaduni wa ukwepaji sheria.