Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afghanistan na mwelekeo wa kutokomeza Polio- WHO

Afghanistan na mwelekeo wa kutokomeza Polio- WHO

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limesema mfumo thabiti wa kufuatilia virusi vya Polio nchni Afghanistan, ndio uti wa jitihada za kutokomeza ugonjwa huo nchini humo wakati huu ambapo visa vipya vimeshuka hadi 13 mwaka jana ikilinganishwa na 20 mwaka 2015.

WHO inasema kwa sasa Afghanistan ina vituo 70 na mtandao wa wafanyakazi wa kujitolea 21,000 wanaofuatilia virusi hivyo hasa vile vikali vinavyosababisha kupooza.

Miongoni mwao ni waganga wa jadi, viongozi wa dini ya kiislamu au Mullah, walinda madhabahu, wataalamu wa dawa.

Akizungumzia jinsi anavyoshiriki katika kutekeleza mfumo huo thabiti, Daktari Saifurrahman amesema anahisi wajibu wa kutokomeza Polio nchini mwake akieleza kuwa ni ugonjwa unaoweza kusababisha kupooza kwa binadamu.

Amesema pindi mgonjwa aliye hatarani kupooza au aliyepooza anapofika kwenye kituo chao, humchunguza kwa kina na iwapo ni dalili za Polio anamhamishia kwa afisa kanda wa Polio ambaye atafanya uchunguzi wa kina zaidi.

Tathmini ya mwaka jana imebaini kuwa mfumo wa ufuatiliaji wa Polio nchini Afghanistani umezidi viwango vya kimataifa na hivyo kuongeza uwezo wa kudhibiti virusi vya Polio.