Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Twalaani ghasia dhidi ya wageni Afrika Kusini- IOM

Twalaani ghasia dhidi ya wageni Afrika Kusini- IOM

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM limeeleza wasiwasi wake kufuatia ghasia dhidi ya wahamiaji kwenye miji ya Johannesburg na Pretoria nchini Afrika Kusini.

Ghasia hizo zimeenda sambamba na mashambulizi, uporaji na uchomaji moto wa mali za wageni ambapo IOM imesema inalaani vikali vitendo hivyo.

Msemaji wa IOM mjini Geneva, Uswisi, Itayi Viriri ameeleza kuwa ni vyema raia wanaokumbwa na matatizo ya kijamii kusaka suluhu kupitia mamlaka husika na si vinginevyo kwa kuwa..

(Sauti ya Itayi)

“Tafiti zilizofanywa nchini Afrika Kusini zinaonyesha kuwa hakuna ushahidi wowote kuwa vitendo vya uhalifu vinatekelezwa na wageni, na badala yake tafiti zinaonyesha kuwa wahamiaji wanaokwenda Afrika Kusini wengi wao hawaathiri fursa za ajira za muda mrefu za raia au mishahara. Wengi wa wageni hufungua biashara ndogo ndogo na walengwa sasa ni wamiliki wa biashara ndogo.”

IOM imesema iko bega kwa bega na Afrika Kusini kushughulikia hali ya sasa ikitolea mfano wa ghasia za mwaka 2008 na 2015 ambapo ilisaidia kurejesha makwao wahamiaji waliotaka kurejea nyumbani.