Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni ya aina yake kulinda bahari yazinduliwa leo #CleanSeas

Kampeni ya aina yake kulinda bahari yazinduliwa leo #CleanSeas

Shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa leo limezindua kampeni ya aina yake yenye lengo la kutokomeza uchafuzi wa bahari utokanao na matumizi holela ya vitu vya nailoni na plastiki ifikapo mwaka 2022.

Uzinduzi umefanyika leo wakati wa mkutano wa viongozi wa juu kuhusu masuala ya bahari huko Bali, Indonesia, kampeni ikilenga matumizi ya plastiki kwenye bidhaa kama vile za urembo hasa zile za kutumika mara moja na kutupa.

Kwa mantiki hiyo kampeni inataka viwanda kupunguza ufungashaji wa bidhaa katika kontena za plastiki ambazo kwazo mteja hutumia mara moja na kutupa na hivyo kusababisha uchafuzi wa mazingira.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Erik Solheim, amesema dunia imechelewa kuchukua hatua akitolea mfano kuwa bidhaa za plastiki zinazotupwa ufukweni huko Indonesia hutwama baharini na kusababisha ongezeko la kina cha bahari ncha ya kaskazini mwa dunia.

Kwa mwaka huu mzima wa 2017, kampeni hiyo iliyopewa jina la #CleanSeas itatangaza mikakati kwa serikali na biashara ili kudhibiti plastiki, ikiwemo kuondokana na bidhaa za matumizi binafsi zilizofungashwa kwenye plastiki, kupiga marufuku au kutoza kodi mifuko ya kutumika mara moja na kupunguza kwa kiasi kikubwa bidhaa za plastiki zisizoweza kutumika zaidi ya mara moja.