Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan yapaswa kulinda haki za raia Darfur-UM

Sudan yapaswa kulinda haki za raia Darfur-UM

Mtaalamu huru wa Umoja wa mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Sudan, Aristide Nononsi, ametoa wito kwa serikali ya nchi hiyo mjini Khartoum kulinda haki za raia kwenye jimbo lililoghubikwa na vita la Darfur.

Bwana Nononsi ametoa wito huo katika mwisho wa ziara yake ya siku 12 ambapo alipata fursa ya kuzungumza na watu wanaoishi katika kijiji cha Adi Kong magharibi mwa Darfur. Amesisitiza jamii ya watu hao bado iko katika hali ya sintofahamu ya usalama na wanahitaji ulinzi wa serikali na huduma za msingi ikiwemo maji elimu, na huduma za afya. Ameongeza kuwa ni muhimu kwa serikali ikisaidiwa na wadau wa kimataifa kulinda haki za raia hao.

Alitembelea pia kambi ya wakimbizi ya Sorotony Kaskazini mwa Darfur na ametoa wito kwa serikali kufanya uchunguzi wa vitendo vyote vya ukiukwaji wa haki za binadamu na kuwafikisha wahusika kwenye mkono wa sheria.

Darfur imekuwa kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2003, na kusababisha maelfu kwa maelfu ya watu kuzikimbia nyumba zao na wengi wao bado wanaishi makambini hadi sasa.