Usalama ni muhimu kuchagiza chanzo kikuu cha chakula Sudan Kusini-UNMISS
Kuimarishwa kwa usalama ni muhimu katika kuchagiza chanzo kikuu cha upatikanaji wa chakula Sudan Kusini amesema mwakilishi wa Katibu Mkuu na mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNMISS Bwana David Shearer.
Bwana Shearer ameyasema hayo baada ya kufanya ziara yake ya kwenza kwenye mji wa Yambio Magharibi mwa jimbo la Equatoria eneo mashuhuri kwa kilimo ambalo limekuwa mzalishaji mkubwa wa chakula kwa ajili ya nchi nzima Sudan kusini.
Hivi sasa uzalishaji umepungua jimboni humo kwa sababu wakulima hawawezi tena kupanda mazao kutokana na vita vinavyoendelea. Kupitia msemaji wa UNIMISS David Shearer ameongeza
(SAUTI YA DANIEL DICKNSON)
“Usalama ni chachu ya kuwarejesha wakulima mashambani kwao, pia amesema kwamba usalama ni muhimu katika mtandao wa barabara ili kuruhusu biashara na usambazaji wa bidhaa za kilimo. Amepongeza uongozi wa jimbo hilo kwa jukumu lao la kuinua uzalishaji wa kilimo na kuelekea katika hali ya kujitosheleza”
Mkuu huyo wa UNMISS amechagiza pia juhudi za upatanishi jimboni humo hususani kuwajumuisha vijana katika jamii ambao wengi wao walijiunga na makundi ya wapiganaji.