Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna mwelekeo chanya kwenye mazungumzo ya Syria: Staffan de Mistura

Kuna mwelekeo chanya kwenye mazungumzo ya Syria: Staffan de Mistura

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria Staffan de Mistura amewaambia waandishi wa habari hivi leo kwamba japokuwa hatarajii suluhisho la haraka kwenye mazungumzo ya amani juu ya Syria yanayoanza hapo kesho mjini Geneva, Uswis na pande zote lakini ana matumaini makubwa juu ya kuendeleza mjadala huo na wahusika.

Amesema kuwa anatarajia mwelekeo chanya kutoka kwa pande mbalimbali kufikia makubaliano.

Wawakilishi wa serikali ya Damascus na upinzani wanakutana Alhamisi mjini Geneva, Uswis chini ya uangalizi kwa msingi wa azimio namba 2254 la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York hii leo ikiwa ni siku moja kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo mwakilishi huyo maalum ameongeza kuwa msingi wa azimio hilo ni mpango wa kimataifa juu ya mchakato wa mpito wa kisiasa ikiwa ni pamoja na kusitishwa kwa mapigano na mengine ni

(Sauti ya Di Mistura)

"Utekelezaji wa utawala bora unaohusisha wote na wakuaminika, la pili ratiba ya uandikishaji na katiba mpya na wenyeji na mpangilio wa uchaguzi sahihi na sawa, chini ya usimamizi wa UM kutekelezwa kwa kiwango cha juu na cha kimataifa. Hii ndio itatoa mwongozo wa majadiliano na pande za Syria."

Bwana Di Mistura ameongeza kuwa mkutano uliofanyika Astana katika makubaliano kati ya Urusi na Uturuki ulipendekeza kusitishwa kwa mapigano na hii imesaidia kuendeleza huo mjadala wa kesho Alhamisi.

(Sauti ya Di Mistura)

"Na hatungeweza kuwa na majadiliano haya bila kusitishwa kwa mapigano. Hii leo mwakilishi wa Urusi kwenye mkutano wa Astana wamenielezea na kutangazia wote kuwa wameitaka rasmi serikali ya Syria kuondoa ndege zao angani na kuwa kimya wakati wa majadiliano ya Geneva. Na tumewaomba walio na ushawishi kwa pande pinzani kujadiliana nao japokuwa hawana ndege lakini kufanya hivyo na kusitisha mapigano."

Kabla ya mwanzo wa mazungumzo hayo hapo Alhamisi, Bwana Di Mistura atakutana na ujumbe wa serikali, wajumbe mbalimbali pamoja na wawakilishi wa kikundi kinachosaidia Syria na kamati .