Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 7 kukwamua familia hitaji Iraq

Dola milioni 7 kukwamua familia hitaji Iraq

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limekaribisha mchango wa dola milioni 7 kutoka Japan ambazo zitatumika kuwapatia chakula familia zilizoathirika na mgogoro huko Mosul nchini Iraq sambamba na wakimbizi wa Syria walio kambini nchini humo.

Akipokea mchango huo, mwakilishi wa WFP nchini Iraq Sally Haydock amesema fedha hizo zinalenga karibu watu 400,000 kwa kuwapatia mgawo wa chakula wa kila mwezi kama vile unga wa ngano, maharagwe, chumvi, mafuta na sukari.

Halikadhalika zitasaidia wakimbizi 65,000 kutoka Syria kwa kuwapatia vocha za pesa ili waweze kununua kile watakacho kutoka maduka yaliyoko maeneo wanamoishi.

Balozi wa Japan nchini Iraq Bwana Fumio Iwai amesema nchi yake ina nia ya kuwasaidia watu wenye mahitaji, hasa raia wa Iraq na wakimbizi wa Syria wanaoishi katika mazingira magumu kutokana na vita huko Mosul kupitia mpango huo ili kukidhi mahitaji yao ya dharura ya chakula.

Fedha hizi za karibuni ni sehemu ya dola milioni 85.2 ambazo WFP imepatiwa ili kuweza kutoa chakula muhimu na msaada wa lishe katika nchi 33 barani Afrika, Asia na Mashariki ya Kati.