Skip to main content

Ingalikuwaje watoto wanaouawa Syria ni wenu? – UNICEF

Ingalikuwaje watoto wanaouawa Syria ni wenu? – UNICEF

Mashauriano baina ya pande kinzani nchini Syria yakianza hii leo huko Geneva, Uswisi, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limetaka washiriki waonyeshe uongozi thabiti kwa kupitisha uamuzi unaoweka mbele haki za watoto wa nchi hiyo wanaokumbwa na mashambulizi kila uchao.

Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya mashariki ya kati, Geert Cappelaere ametolea mfano mtoto wa kiume ambaye alipoteza miguu yake yote miwili kwenye shambulio huko Idlib wiki iliyopita akihoji wahusika ingalikuwa vipi kama watoto hao wangalikuwa ni wa kwao.

Amesema tangu mwaka huu uanze watoto 20 wameuawa kwenye mashambulio, wengine wengi wakijeruhiwa akiwemo mtoto mchanga ambaye alijeruhiwa nyumba yao ilipopigwa kombora kwenye viunga vya mji mkuu Damascus.

Bwana Cappalaere amesema sitisho la mapigano bado halijaepusha watoto na kwamba gharama wanayolipa watoto kutokana na mzozo huo ni aibu kwa dunia na hivyo hatua zichukuliwe kusaka suluhu ya kisiasa.

Ametaka pande zote kwenye mzozo wa miaka sita sasa na wale wenye ushawishi kuchukua hatua kutokomeza mapigano.