Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nigeria yahitaji dola bilioni 1 kuokoa maisha ya mamilioni ya watu: OCHA

Nigeria yahitaji dola bilioni 1 kuokoa maisha ya mamilioni ya watu: OCHA

Wakati mashirika ya misaada yakiongeza kasi ya huduma za kibinadamu Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, msaada wa dola zaidi ya bilioni moja unahitajika ili kuokoa maisha ya mamilioni ya watu walioathirika na ghasia za Boko Haram limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA.

Endapo fedha hazitowasili kwa wakati basi mtoto mmoja kwati ya watano wanaougua utapia mlo uliokithiri wanaweza kupoteza maisha , amesema Peter Lundberg, naibu mratibu wa masuala ya kibinadamu nchini Nigeria

Kwa mujibu wa OCHA mgogoro wa miaka minane nchini humo umewaacha watu milioni 8.5 wakihitaji msaada wa kibinadamu hasa katika maeneo yaliyoathirika zaidi ya Kaskazini Mashariki mwa nchi.

Pia shirika hilo limesema katika miezi ijayo watu wapatao milioni 5.1 watakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula katika eneo hilo ambako tyayari watu zaidi ya milioni moja wametawanywa na machafuko na wengine wengi wakikabiliwa na vita na ukatili.