Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunaazimia kukomboa maeneo 17 kutoka ukoloni- Guterres

Tunaazimia kukomboa maeneo 17 kutoka ukoloni- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo amehutubia kikao cha kwanza cha kamati maalum ya Baraza Kuu la Umoja huo kuhusu kupatia uhuru nchi ambazo bado zinatawaliwa na kusisitiza umuhimu wa kamati hiyo katika kufanikisha nchi zote zilizo chini ya ukoloni zinapata uhuru.

Amesema anafahamu machungu ya kutawaliwa akielezea uzoefu wake wakati wa makuzi huko Ureno akisema udikteta wa António de Oliveira Salazar nchini humo ulikandamiza demokrasia lakini hatimaye nchi ilipata uhuru baada ya jeshi kuchoshwa na udhalimu.

Katibu Mkuu amesema kamati imepata mafanikio kusaidia ukombozi wa nchi akisema wakati inaanzishwa mwaka 1962, Umoja wa Mataifa ulikuwa na wanachama 110 na sasa kuna wanachama 193 na idadi kubwa ya wanachama wapya walikuwa makoloni.

Hata hivyo amesema…

(sauti ya Guterres)

“Licha ya mafanikio hayo makubwa, bado maeneo 17 yanatawaliwa. Tunataka kusisitiza azma ya kamati hii maalum kusaidia kila eneo kupata muundo na muda wake wa kukamilisha harakati za kujikwamua na ukoloni kwa kuzingatia mazingira ya kila eneo.”