Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfuko wa UM watoa dola milioni 18.5 kusaidia Ethiopia

Mfuko wa UM watoa dola milioni 18.5 kusaidia Ethiopia

Wakati Pembe ya Afrika ikikabiliwa na moja ya ukame mbaya kabisa kwa miongo kadhaa , zaidi ya watu milioni 5.6 nchini Ethiopia wanahitaji haraka msaada wa mahitaji ya lazima.

Shirika la Umoja wa mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na msaada wa dharura OCHA limesema ili kutoa kwa wakati msaada muhimu unaohitajika kwa zaidi ya watu 785,000 wanaokabiliwa na njaa, utapia mlo na ukosefu wa maji kwenye jimbo la Somalia nchini Ethiopia, mratibu wa misaada ya dharura na msaididizi wa Katibu mkuu katika masuala ya kibinadamu Stephen O’Brien ametoa dola milioni 18.5 kutoka kwenye mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa CERF . Jens Learke msemaji wa OCHA anafafanua zaidi.

(Sauti ya Jens Learke)

"Fedha hizo zitasaidia takriban watu 785,000 wanaokabiliwa na njaa, utapiamlo na uhaba wa maji katika eneo la Somali nchini Ethiopia, eneo ambalo limeathirika vibaya na ukame. Kwa jumla kuna watu karibu milioni 5.6 Ethiopia ambao ni wahanga wa ukame uliokithiri ambao unashuhudiwa eneo zima la pembe ya Afrika."