Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wapiganaji zaidi ya 300 wa FARC-EP nchini Colombia waweka chini silaha

Wapiganaji zaidi ya 300 wa FARC-EP nchini Colombia waweka chini silaha

Karibu wapiganaji 300 waliobaki wa jeshi la mapinduzi au FARC-EP nchini Colombia wamewasili katika kituo cha Agua Bonita, Colombia ya kati ili kuweka chini silaha zao. Hiyo ni kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini humo ambapo timu ya waangalizi wa kimataifa wanafuatilia kusitishwa kwa mapigano nchini humo na pia mchakato wa kuondoa na kupokea silaha hizo.

Mgogoro kati ya vikosi vya serikali na waasi umedumu kwa zaidi ya miaka 50, ambapo zaidi ya watu 260,000 walipoteza maisha kabla ya kutiwa saini mkataba mpya wa amani  mwezi Novemba mwaka jana.

Taarifa hiyo ya Umoja wa Mataifa pia imethibitisha kuwa karibu wapiganaji 7,000 wanachama FARC-EP wamewasili katika maeneo ya kanda ili kuanza maisha ya kiraia,  na chini ya mkataba huo wa amani wana wajibu wa kukusanyika katika maeneo 27 ili kusalimisha silaha.

Serikali ya Colombia ndio imesimamia vifaa vyao kwenye kambi na mahitaji ya familia zao.

Naye naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq amesema kuwa katika kipindi cha siku 19, wapiganaji hao wakiwemo wanaume na wanawake, baadhi yao waja wazito au wana watoto wadogo, wametumia magari, mabasi, boti au kutembea kufikia maeneo 36 kote nchini. Mkuu wa waangalizi wa ujumbe huo Kamanda Javier Pérez Aquino, amesema kuwa uamuzi  huo wa FARC-EP ni mzuri na ana matumaini kwamba kuwepo kwa waasi hao wa  zamani kutaharakisha kazi ya ujenzi katika kambi hizo.