Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zeid ametoa wito kusitishwa kwa mauaji mara moja DRC

Zeid ametoa wito kusitishwa kwa mauaji mara moja DRC

Kamishna mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein ameitaka serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuchukua hatua za haraka kusitisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja mauaji ya raia yanayofanywa na jeshi la nchi hiyo. Amesema kuna habari za kuaminika na madai ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika eneo la Kasai kati na mashariki na jimbo la lomami, huku kukiwa na kuzorota kwa kasi hali ya usalama huku watu wakilengwa na askari kwa madai ya uhusiano na wanamgambo wa ndani.

Kamishna Zeid ametoa wito kukabiliana na mzizi ya mgogoro kati ya serikali na wanamgambo badala ya kuwalenga raia wakidhaniwa kuwa ni wanamgambo. Ametaja kuwa sambamba na majukumu yake ya kimataifa ya haki za binadamu, serikali ya DRC lazima ihakikishe kuwa vikosi vyake vya usalama, ikiwa ni pamoja polisi na jeshi, vina heshimu na kulinda maisha ya raia.

Inadaiwa kuwa wanamgambo wanaohusishwa na chifu wa kitamaduni Kamuina Nsapu, ambaye aliuawa na majeshi mnamo Agosti 2016 wamekuwa wakifanya vurugu kwenye eneo hilo la Kasai kwa kushambulia majengo ya serikali na makanisa, na vikosi vya usalama wa taifa.

Ripoti hiyo pia inadai kutumiwa kwa watoto kwenye mzozo. Pia kuna video ambayo haijadhibitishwa inayoonyesha askari wa FARDC wakiwafyatulia risasi nyingi wanaume na wanawake bila ya onyo wakidai kuwa ni wa kundi la wanamgambo wa Kamiuna Nsapu, kijijini Muenza Nsapu, japokuwa msemaji wa serikali na waziri wa mawasiliano wa DR Congo Lambert Mende amesema kuwa uchunguzi unafanywa dhidi ya maafisa wa FARDC kufuatia madai hayo.

Kamishna Zeid ametoa wito tena kwa serikali kuongeza jitihada zake za kukabiliana na ukatili unaoleta ukiukwaji wa haki za binadamu.