Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Migogoro yaielemea dunia, suluhu ni diplomasia ya amani : Guterres

Migogoro yaielemea dunia, suluhu ni diplomasia ya amani : Guterres

Akiwa ziarani nchini Ujerumani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres  amezungumza katika mkutano kuhusu usalama mjini Munich ambapo amesema migogoro duniani ni tishio hususani mtindo mpya ambapo wapiganaji huhama kutoka nchi moja kwenda nyingine.

Guterres  amesema amani ya dunia iko shakani, kwani migogoro huvuka mipaka akitolea mfano ya Nigeria, Mali, Libya, Yemen, Syria na nchi nyigine za  Mashariki  ya Kati.

Amesema suluhu  inahitaji nchi husika katika kukabiliana na ugaidi na kwamba.

( Sauti Guterres)

‘Haitakuwa rahisi, tutahitaji kiwango kikubwa cha diplomasia ya kuzuia, na juhudi nyingi katika upatanisho. Tunahitaji mkakati maalum wa kukabiliana na chanzo cha aina hii ya migogoro duniani.’’

Amesema Umoja wa Mataifa unajihusisha katika maeneo matatu ya mabadiliko ya chombo hicho ambayo ni mkakati wa amani na usalama, mfumo wa operesheni na usanifu, yote hayo yakilenga katika kuwekeza rasilimali katika kuzuia migogoro na kulinda amani. Akijibu maswali ya wanahabari, Guterres amezungumzia mambo mseto ikiwamo utekelezaji wa maendeleo endelevu akitaka nchi zisaidiwe kukuza rasilimali zao akizungumzia mabadiliko katika mfumo wa kodi.

Kuhusu Syria,  amesema suluhu ya mgogoro huo pamoja na mambo mengine unahitaji utashi wa pande kinzani na kwamba.

( Sauti ya Guterres)

‘‘Na pia nafikiri ni muhimu kusema kuwa hakuna namna tunaweza kushinda dhidi ya Daesh kama hatuwezi kutafuta suluhisho jumuishi kwa ajili ya Syria na kwa Iraq.’’

Kuhusu zuio la Marekani dhidi ya pendekezo la Salam Fayyad kutumika kama Mwakilishi wa  Katibu Mkuu nchini Libya amesema.

(Sauti ya Guterres)

‘‘ Kama nilivyosema mara kadhaa. Nadhani ilikuwa kosa kubwa. Nadhani Bwana Fayyad alikuwa mtu sahihi katika wakati sahihi kwa wakati sahihi na watakaoumia ni watu wa Libya na mchakato wa amani wa Libya.’’