Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Radio na Teknolojia hususan Burundi

Radio na Teknolojia hususan Burundi

Wiki hii tarehe 13 mwezi wa Februari, dunia imeadhimisha siku ya Radio duniani, ujumbe ukiwa Radio ni wewe! Ujumbe huu mahsusi umezingatia vile ambavyo chombo hicho chenye jukumu la kuelimisha, kuburudisha na kuhabarisha kinavyomshirikisha msikilizaji kutwa, kucha na popote pale alipo.

Waandaaji wa vipindi hubonga bongo kuhakikisha msikilizaji anakuwa sehemu ya matangazo hayo na kukidhi mahitaji yao ya kiuchumi, kijamii na kisiasa, huku wabobezi wa teknolojia nao wakihaha kuhakikisha kuwa teknolojia haiachi nyumba matunda ya chombo hicho.

Ni kwa muktadha huo, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO, Irina Bokova amesema kuwa radio haijawahi kuwa muhimu wakati wowote ule kuliko hivi sasa kwenye maendeleo ya sayansi na teknolojia. Mabadilishano ya taarifa mbali mbali kupitia mbinu mbali mbali yamefanya Radio nayo kwenda na wakati.

Ni kwa muktadha huo huo amesema ni lazima kuhaha kuhakikisha radio katika zama hizi inafanikisha utekelezaji wa ajenda ya maendeleo endelevu, SDGs ifikapo mwaka 2030. Hata hiyo baadhi ya watu wanadai kuwa maendeleo ya teknolojia yanaweza kuacha nyuma Radio. Je hali ikoje nchini Burundi? Mwandishi wetu wa Maziwa Makuu, Ramadhani Kibuga amevinjari na kutuletea taarifa hii.