Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni moja shakani Ukraine-UNICEF

Watoto milioni moja shakani Ukraine-UNICEF

Mgogoro nchini Ukraine ukiingia mwaka wa nne, watoto milioni moja wako katika uhitaji wa dharura wa kibinadamu ikiwa ni idadi mara mbili ikilinganishwa na mwaka jana, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF.

UNICEF imesema Ongezeko hilo la wasichana na wavulana 420,000 linatokana na kuendelea kwa mapigano na kuzorota kwa maisha Mashariki mwa taifa hilo, ambapo zaidi ya watu milioni moja na nusu ni wakimbizi wa ndani, familia nyingi zimepoteza vipato, mafao ya kijamii na huduma za afya huku bei za bidhaa zikipanda.

Shirika hilo limesema hii ni dharura isiyoonekana na iliyosahaulika, huku watoto nchini Ukraine wakiishi katika vitisho mfululizo kwa miaka mitatu iliyopita kwani shule zao zimeharibiwa, wamelazimishwa kutoka majumbani kwao na mahitaji yao muhimu kama vile malazi, joto katika msimuwa baridi na maji vimetoweshwa.

Christophe Boulierac ni msemaji wa UNICEF Geneva.

(Sauti ya Boulierac)

‘‘UNICEF kwa mara nyingine inatoa wito kwa pande zote kusitisha mapigano hima na kwa mujibu wa mkataba wa Misk uliosainiwa mwezi Agosti mwaka 2015 na kuitikia wito wa sheria ya kimataifa ya usaidizi wa kibinadamu , ikiwemo kuruhusu ufikishwaji wa misaada katika maeneo ulipozuiwa.’’