Skip to main content

Manusura katika mgogoro Ukraine watelekezwa-UM

Manusura katika mgogoro Ukraine watelekezwa-UM

Manusura wa ukatili wa kingono kwenye machafuko nchini Ukraine mara nyingi wananyimwa haki au wanaachwa bila msaada wanaostahili na ushauri nasaha suala linalowafanya kuwa wahanga mara mbili kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyochapishwa leo.

Ripoti hiyo yenye kurasa 37 iliyoandaliwa na ujumbe wa umoja huo ya kufuatilia haki za binadamu nchini Ukraine inasema kwamba mfumo wa taifa hilo unakosa sheria, uwezo na wataalamu wenye uzoefu wa kuchunguza kikamilifu na kuendesha mashtaka dhidi ya uhalifu wa kingono unaosambazwa kutokana na ukwepaji wa sheria kwa watekelezaji.

Nataliya Pylypiv ni mwandishi mkuu wa rpoti hiyo na afisa wa haki za binadamu.

(Sauti Nataliya)

"Kulikuwa na kupigwa na kufinywa sehemu za siri kutumia vifaa vya umeme, ukatili wa kijinsi na kuvuliwa mavazi kwa lazima, ukatili wa aina hizi zote ulitumika kama sehemu ya mateso na ukadamizaji kama mbinu ya kutoa taarifa."

Mmoja wa manusura katika ripoti hiyo amenukuliwa akilalama ‘’Kwanini kusema nini kilichonitokea? Hakuna atakayenisadia na hakuna atakayeweza kuwapata waliotekeleza . Hakuna atakayewaadhibu.’’

Visa vingi katika ripoti ambayo ni ya kipindi cha Machi 14 mwaka 2014 hadi Januari 31 mwaka huu, vilitokea wakati watu hao walipowekwa kizuizini na vikosi vya serikali au waasi.

Ripoti imehusisha maeneo ya Ukraine na Jamhuri ya Crimea hususani kanda za Mashariki ambazo ziko chini ya vikosi vyenye silaha.