Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku zijazo kuna uwezekano wa chakula kupatikana baharini zaidi kuliko nchi kavu

Siku zijazo kuna uwezekano wa chakula kupatikana baharini zaidi kuliko nchi kavu

Endapo jumuiya ya kimataifa itaweza kudhibiti uvuvi uwe endelevu zaidi , basi chakula katika siku za usoni kina uwezekano wa kupatikana baharini zaidi kuliko nchi kavu.

Kauli hiyo ni kwa mujibu wa Kim Friedman, afisa wa maliasili na uvuvi katika shirika la chakula na kilimo FAO.

Alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa maandalizi wa masuala ya bahari unaoendelea kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York wiki hii , kabla ya mkutano mkubwa wa Juni, ambao utajadili jinsi gani viumbe vya baharini vinaweza kulindwa na kuwa endelevu katika miongo ijayo.

Bwana Friedman amesema uvuvi wa kupita kiasi inamaanisha hasara katika uzalishaji ya takribani tani milioni 16.5, lakini ni vigumu kupima athari za uvuvi haramu na uvuvi holela. Bwana Friedman anaeleza ni kwa nini mkutano huu wa siku mbili unaohusisha nchi wanachama na asasi za kiraia ni muhimu.

(SAUTI YA FRIEDMAN)

“kumekuwa na utambuzi na imani ya kawaida kwamba changamoto baharini ni kubwa , hata hivyo tunahitaji kutambua wapi tunafanya vizuri na maeneo ambayo hatufanyi vizuri , na jinsi gani tunaweza kuleta pamoja nguvu za kila mtu ili kujikita katika tatizo moja, na unaweza kufikiria kama mashirika mengi yanavyojitahidi kufanya mambop yanayohitajika , kuna matatizo tata huko.”