Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunataka habari za wakimbizi 20,000 waliokimbia Wau Shilluk

Tunataka habari za wakimbizi 20,000 waliokimbia Wau Shilluk

Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, David Shearer, amesema ukosefu wa habari kuhusu wakimbizi wa ndani 20,000 kwenye ukingo wa magharibi wa mto Nile nchini humo ni tatizo kubwa. Flora Nducha na taarifa kamili

(TAARIFA YA FLORA)

Bwana Shearer ambaye alizuru eneo hilo kwa mara ya kwanza baada ya kuchukua wadhifa wake wiki nne zilizopita amesema, mapigano ya hivi karibuni kati ya jeshi la serikali la SPLA na lile la upinzani yamepanuka kijiografia katika ukingo wa magharibi na hakuna dalili za mabadiliko, na hilo limelazimu watu zaidi kukimbia makazi yao.

Amesema kitendo cha SPLA kuzuia walinda amani wa UNMISS kufanya doria katika eneo la Wau Shilluk, ili kufahamu habari za wakimbizi 20,000 wanosadikiwa kukimbia eneo hilo, ni jambo la kubughudhi, kama ujumbe wake unavyowasilishwa na msemaji wa UNMISS Daniel Dickinson

(Sauti ya Daniel)

"Tunataka kujua kilichotokea kwa watu hao, na kuwapatia msaada ikiwa wanauhitaji".

Wakati huo huo UNMISS imesema katika kipindi cha wiki moja sasa, Uganda inapokea takriban wakimbizi 4,000 kila siku, wengi wao wanawake na watoto kutoka eneo la Kajo Keji Sudan Kusini