Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hofu yaongezeka kuhusu mkwamo wa majadiliano ya kisiasa DRC

Hofu yaongezeka kuhusu mkwamo wa majadiliano ya kisiasa DRC

Jumuiya ya kimataifa ikiwemo Muungano wa Afrika AU, Umoja wa Mataifa, Muungano wa Ulaya EU na shirika la kimataifa  la nchi zinazozungumza  Kifaransa IOF imesema inatiwa hofu na kuendelea kwa mkwamo kwenye mjadiliano ya kisiasa miongoni mwa wadau nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kuhusiana na utekelezaji wa mikakati ya makubaliano ya kisiasa yaliyoafikiwa Desemba 31 mwaka jana. Taarifa kamili na John Kibego.

(Taarifa ya Kibego)

Mashirika hayo manne yamesema yamebaini kwamba wiki sita baada ya makubaliano ya kipindi cha mpito ili kuelekea kufanya uchaguzi huru wa amani na haki Desemba 2017, pande husika bado hazijakamilisha majadiliano ya utekelezaji wa mkataba.

Na kuongeza kuwa hali hiyo inaweza kutia dosari nia njema iliyosababisha kutiwa saini makubaliano mwezi Desemba mwaka jana.

Hivyo mashirika hayo yametoa wito kwa wadau wote nchini DRC ikiwa ni pamoja na upande wa serikali na wapinzani kuongeza mara mbili juhudi kwa nia njema ili kuharakisha na kukamilisha majadiliano yanayoendelea , kwani wamesema kuna haja ya pande zote kushikamana katika mchakato wa upatanishi na kuhakikisha makubaliano ya 31 desemba yanatekelezwa kwani ni muhimu sana kabla ya uchaguzi.