Skip to main content

Kenya yaonywa kukomesha ukandamizaji kwa asasi za kiraia kuelekea uchaguzi mkuu Agosti-UM

Kenya yaonywa kukomesha ukandamizaji kwa asasi za kiraia kuelekea uchaguzi mkuu Agosti-UM

Wataalam maalum watatu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wametoa wito kwa serikali ya Kenya kusitisha ukandamizaji kwa mashirika ya kiraia ambao umezidi wakti huu ikielekea kwenye uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.

Kwa mujibu ya taarifa yao ya pamoja kutoka Geneva, Uswisi wataalamu hao wamesema wana wasiwasi mkubwa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya mashambulizi dhidi ya vyama vya kiraia wakati uchaguzi ukikaribia.

Wataalam hao Maina Kiai anayehusika na uhuru wa kujumuika na kukusanyika kwa amani, David Kaye wa  haki ya uhuru wa kutoa maoni na kujieleza na Michel Forst anayehusika na  haki ya watetezi wa haki za binadamu wamesema inaonekana kuna utaratibu wa makusudi wa kukandamiza mashirika ya kiraia yanayojadili sera za serikali, kuelimisha wapiga kura, kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu na masuala ya rushwa. Masuala haya ni muhimu sana katika demokrasia, na kujaribu kuzima mjadala huo katika nafasi ya kiraia inatishia uhalali wa uchaguzi ujao wameongeza wataalamu hao..

Wataalam hao pia wamegusia juu ya hoja ya serikali iliyosambazwa hivi karibuni inayotishia kufungwa kwa mashirika yasiyo ya kiserikali yasiyo na leseni sahihi kwa madai kwamba ni tisho kwa usalama wa taifa, matumizi wa fedha chafu na matumizi ya misaada ya wafadhili na ufadhili wa ugaidi ikiwemo pia kutishia tume ya haki za binadamu ya kitaifa.

Pia wameikosoa serikali kwa kushindwa kutekeleza kifungu cha sheria juu ya faida ya umma iliyosainiwa Januari 14, 2013, na haijawahi kutekelezwa. Sheria inalenga kutoa mazingira bora kwa mashirika hayo. Wameongeza kuwa haki ya uhuru wa kushirikiana ni muhimu katika mazingira ya kabla ya uchaguzi, ambapo wapiga kura wana wajibu wa kuchagua wawakilishi wao na kupewa nafasi na mazingira bora kuitimiza haki hiyo.