Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya Ukreni bado ni tete huku usitishaji uhasama ukikiukwa: UM

Hali ya Ukreni bado ni tete huku usitishaji uhasama ukikiukwa: UM

Ongezeko la mapigano kati ya waasi wanaounga mkonoUrusi na majeshi ya Ukraine karibu na maeneo yenye wakazi wengi mashariki mwa nchi hiyo kunahatarisha maisha ya raia, amesema mwakilishi mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini humo akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva hivi leo.

Bwana Neal Walker ambaye pia ni mratibu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa kuongezeka na kuwepo kwa silaha nzito ni ishara kuwa mapigano yanaweza kuanza tena wakati wowote.

Ameongeza kuwa kulikuwa na mapigano makali sana Januari 21 hadi Februari 3 ambapo ukiukaji wa kusitisha mapigano umefanyika  zaidi ya mara 30,000.

Mratibu huyo mkazi wa UM ameelezea hali ya kibinadamu nchini humo ni muhimu kuitilia maanani, huku hali ya majira ya baridi ikiendelea. Pia ameonya kuhusu uharibifu wa mazingira na miundombinu muhimu ya raia kutokana na makombora yanayolipuliwa akitoa mfano wa mtambo wa kemikali ya fenoli ambayo inayoweza kufanya uharibifu mkubwa wa mazingira ikiwa utaendelea kutupiwa makombora na kuharibiwa zaidi.

Tangu mwanzo wa mgogoro huo Aprili 2014, karibu watu 10,000 wameuawa na tayari kuna karibu wakimbizi wa ndani kati ya 800,000 huku wengine millioni moja  wakiwa katika maeneo ya serikali. Inakadiriwa kuwa karibu wakimbizi 200,000 wako  kwenye maeneo yasiyo ya serikali.