Mlipuko wa homa ya manjano DRC wamalizika- WHO

Mlipuko wa homa ya manjano DRC wamalizika- WHO

Shirika la afya ulimwenguni WHO limetangaza kumalizika kwa mlipuko wa homa ya manjano huko Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, nchi hiyo ikiungana na Angola ambayo nayo ilitangaza kutokomeza ugonjwa huo mwezi disemba mwaka jana.

Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti amepongeza hatua hiyo hiyo iliyotokana na uratibu wa aina yake baina ya taasisi za serikali, wahudumu wa afya na wadau akisema ugonjwa huo ulitikisa nchi mbili hizo kwa kipindi cha miezi sita iliyopita.

Hatua hizo ni pamoja na chanjo dhidi ya homa ya manjano kwa watu zaidi ya milioni 30 huko DRC na Angola, chanjo zilizotolewa kupitia kampeni za dharura zilizoanzishwa.

Nchini Angola visa 884 vilithibitishwa kuwa ni homa ya manjano ambapo wagonjwa 121 walifariki dunia ilhali huko DRC kati ya visa 81 vilivyothibitishwa, watu 16 walifariki dunia.