Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DPRK ikishutumiwa kwa jaribio, yenyewe yasema ina haki ya kujilinda

DPRK ikishutumiwa kwa jaribio, yenyewe yasema ina haki ya kujilinda

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limealaani vikali kitendo cha hivi karibuni cha Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK kurusha kombora la masafa marefu.

Wajumbe wa baraza hilo wamesema kitendo hicho ni kinyume na maazimio ya baraza na kwamba kinadhihirisha mpango wa DPRK kuendeleza mifumo ya kusafirisha silaha za nyuklia.

Wamesema kinachosikitisha zaidi, nchi hiyo badala ya kutumia rasilimali zake kuboresha maisha ya watu wake, inazitumia kuimarisha mifumo ya silaha.

Hata hivyo huko Geneva, Uswisi hii leo wakati wa mkutano wa kupinga kuenea kwa silaha, DPRK imepinga shutuma za jamii ya kimataifa juu ya hatua yake hiyo ya hivi karibuni.

Mwakilishi wa DPRK kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa huko Geneva, Han Tae Song amesema nchi yake inahisi kuwa inakabiliwa na kitisho hivyo ina haki ya kujilinda.