Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MINUSCA kuendelea kutoa ulinzi wa raia nchini CAR

MINUSCA kuendelea kutoa ulinzi wa raia nchini CAR

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, umesema unaendelea na wajibu wake wa kutoa ulinzi kwa raia kwa idhini na ombi la serikali ya nchi hiyo na kwa mujibu wa mamlaka yake yaliyowekwa na maazimio ya Baraza la usalama.

MINUSCA imesema itaendelea pia kuimarisha eneo la Ouaka, ambako kumekuwa na mapigano kati ya vikundi viwili cha FPRC na UPC na kusababisha watu 20,000 kukimbia makwao huku wafanyikazi wa misaada wakizuiliwa kuingia katika maeneo ya Bria na Bambari.

Taarifa hiyo ya MINUSCA imemnukuu msemaji wake Vladimir Monteiro akisema wataendelea kutekeleza majukumu bila upendeleo, kwa lengo la kupunguza kuwepo kwa tishio la makundi ya waasi nchini humo na kutumia njia zote ili kuchagiza kwa azimio la amani kwa pande zinazozozana.

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa ujumbe wa MINUSCA amesema ataendelea na juhudi zake za kujadiliana na pande zote akisisitiza kwamba ni lazima amani ipatikane kwa njia ya mazungumzo akisisitiza kuwa  hakuna sababu zinazoweza kuhalalisha umwagikaji wa damu ya wasio na hatia.

MINUSCA imekumbusha makundi ya waasi kuwa mashambulizi yoyote kwa vikosi vya kimataifa, wafanyi kazi wa Umoja wa Mataifa na watendaji wa kibinadamu ni uhalifu wa kivita ambao unaweza kushitakiwa kwenye mahakama za ndani na za kimataifa.