Sera za chuki dhidi ya uislamu huchochea ugaidi: Guterres

Sera za chuki dhidi ya uislamu huchochea ugaidi: Guterres

Katika dunia ya leo ugaidi unaletwa na mambo mengi, zaidi ikiwa ni ukosefu wa ufumbuzi wa kisiasa katika nchi kama vile nchini Syria pamoja na sera za chuki dhidi ya uislamu.

Hiyo ni kauli ya Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres aliyotoa leo kwenye mkutano na waandishi wa habari, mjini Riyadh, baada ya mazungumzo yake na waziri  wa mambo ya nje wa Saudi Arabia, Adel bin Ahmad Al-Jubeir.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari uliohudhuriwa na Waziri Al-Jubeir, Bwana Guterres amesema kauli za chuki na hisia kinzani dhidi ya uislamu huchochea propaganda za vikundi vyenye misimamo mikali kama vile ISL au Da'esh.

Amesema kinachohitajika ni mbinu thabiti za kupambana na ugaidi ikiwemo kuweka mazingira kwa jamii za makabila tofauti, dini na tamaduni ziwe jumuishi na zitangamane na hivyo kufanya utofauti kuwa ni utajiri badala ya tishio.

Guterres ameishukuru Saudi Arabia kwa jinsi inawezesha kuleta pamoja vikundi kinzani nchini Syria huku akisema ana imani kuwa mkwamo wa mazungumzo nchini Yemen unaweza kupatiwa suluhu na mazungumzo yakaanza upya.