Skip to main content

Baraza la usalama lalaani kuendelea kwa mapigano Sudan Kusini

Baraza la usalama lalaani kuendelea kwa mapigano Sudan Kusini

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani vikali kuendelea kwa mapigano nchini Sudan Kusini hususani katika ukanda wa  Equatoria na Upper Nile, na kutaka kukomeshwa kwa uhasama mara moja.

Taarifa ya baraza hilo ya kulaani mapigano hayo imesema, baraza limelaani vikali mashambulizi dhidi ya raia na kueleza kusikitishwa kwake kwamba kwa mara nyingine kuna ripoti za mauaji dhidi ya raia, ukatili wa kingono na kijinsia, uharibifu wa nyumba, machafuko ya kikabila, pamoja na uwizi wa mifugo na mali nyingine.

Wajumbe wa baraza la usalama wametaka serikali ya mpito  ya umoja wa kitaifa, kuchukua hatua kuhakikisha wanaohusika na mashambulizi hayo wanawajibishwa, na kadhalika kuelezea kusikitishwa kwao kufutia zaidi ya watu 84,000 kukimbia Sudan Kusini tangu mwanzo wa mweiz Januari huku wengi wakiendelea kufurushwa.

Wamesisitiza umuhimu wa suluhu kwa njia ya mchakato wa kisiasa, na kwamba hakuna suluhu ya kijeshi kwa mgogoro huku wakiwakumbusha pande kuwa isitishwaji wa mapigano ni muhimu kwa mafanikio ya ujumuishwaji wa mchakato wa kisiasa, ikiwemo majadiliano ya kitaifa

Wajumbe wa Baraza la Usalama wametoa wito kwa wadau wote wa kutekeleza makubaliano ya amani yaliyoandaliwa na Muungano wa Afrika mwaka 2015 ambayo inategemea mjadala wa kitaifa kwa pande zote na jitihada kubwa za kimataifa.