Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres na Erdoğan wajadili Syria na Iraq

Guterres na Erdoğan wajadili Syria na Iraq

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres aliyeko ziarani nchini Uturuki amekuwa na mazugumzo na Rais Recep Tayyip Erdoğan mjini Istanbul ambapo pamoja na kushukuru nchi hiyo kwa kuhifadhi wakimbizi wamejadili pia mizozo mashariki ya kati.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imetaja mathalani hali nchini Syria na jitihada za kidiplomasia zinazoendelea za kumaliza mgogoro huo.

Katibu Mkuu ameshukuru kuwa mkutano wa hivi karibuni huko Astana, Kazakhstan kuhusu Syria ambao pia Uturuki ni mratibu, umefanyika kwa muktadha wa mazungumzo ya Geneva kuhusu Syria.

Amesisitiza umuhimu wa kukabiliana na ugaidi na wenye misimamo mikali nchini Syria, lakini akisema kuwa harakati hizo hazitafanikiwa bila suluhu ya kisiasa inayoungwa mkono na wananchi.

Wamezungumzia pia harakati za kunasua mji wa Mosul nchini Iraq kutoka magaidi na wenye msimamo mkali akisema harakati hizo zisifanyike kwa misingi ya kidini bali kwa misingi ya maridhiano ya kitaifa.