Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usaidizi wa haraka wahitajika Yemen: UNICEF, FAO, WFP

Usaidizi wa haraka wahitajika Yemen: UNICEF, FAO, WFP

Kadri janga la ukosefu wa chakula linavyozidi kushika kasi nchini Yemen, mashirika ya Umoja wa Mataifa yametoa wito wa dharura kukabiliana na hali hiyo.

Tathmini  ya pamoja ya chakula na lishe iliyofanywa na mashirika hayo, lile la chakula na kilimo, FAO, mpango wa chakula, WFP na lile la kuhudumia watoto, UNICEF, inaonyesha kuwa idadi ya watu wanaokabiliwa na uhaba wa chakula nchini humo imeongezeka kwa miezi saba na kufikia milioni 3.

Hii ni tathmini ya kwanza ya kitaifa na kwenye kaya nchini tangu ongezeko la migogoro katika  mwezi Machi mwaka 2015.

Katika hatua nyingine Kamishna wa haki za binadamu, Zeid Ra'ad al-Hussein, ametoa wito kwa pande zinazopigana nchini Yemen kuheshimu maisha ya raia waliozingirwa kwenye mji wa bandari wa Al Moham, katika jimbo la Taiz.

Msemaji wa ofisi ya ya haki za binadamu Rupert Colville amemnukuu Bwana Zeid akisema taarifa walizopokea zinaonyesha kwamba raia wanalengwa, sambamba na miundombinu katika wiki mbili za mashambulizi.

(Sauti ya Colville)

"Tayari nchi inaweza kujikuta hatarini na kusaka misaada ya dharura ya kibinadamu ikiwa bandari ya Al-Hudaidah ambayo ndio mojawapo ya kuingiza misaada ya kibinadamu itaharibiwa. Na Umoja wa Mataifa umesema kuwa takriban watu milioni 12 wana uhaba wa chakula, watu milioni 3.3 na watoto 2.1 wana utapiamlo. Raia wa Yemen wanajikuta kwenye mgogoro mgumu ulionzishwa na watu, na wanaendelea kuishi kwa uoga na kwenye njaa."