Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya wakimbizi Sudan Kusini yazidi kupaa- UNHCR

Idadi ya wakimbizi Sudan Kusini yazidi kupaa- UNHCR

Idadi ya raia wa Sudan Kusini waliosaka hifadhi nje ya nchi yao kutokana na mapigano yanayoendelea imevuka milioni 1.5 na hivyo kutia wasiwasi mkubwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.

UNHCR inasema idadi hiyo ni kando ya wale zaidi ya milioni mbili ambao ni wakimbizi wa ndani hivyo linatoa wito kwa pande kinzani kusaka haraka suluhu ya amani kwenye mzozo huo ulioanza mwezi disemba mwaka 2013.

Willliam Spindler ambaye ni msemaji wa UNHCR huko Geneva, Uswisi amesema kutokana na idadi hiyo kubwa ya wakimbizi, Sudan Kusini ndio inayotoa wakimbizi wengi barani Afrika na duniani ni ya tatu baada ya Syria na Afghanistan, hivyo anasema..

(Sauti ya William)

“Tunatoa wito kwa pande zote husuka kwenye mzozo kusaka suluhu ya amani kwenye mzozo huo. Bila suluhu, maelfu ya raia wataendelea kuwasili kila siku nchi jirani na Sudan Kusini kama vile Uganda, Ethiopia, Sudan, Kenya, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, na Jamhuri ya Afrika ya Kati wakati huu ambapo huu ni mwaka wanne.”

Wakimbizi waliowasili hivi karibuni wanasimulia kuwepo kwa mapigano makali nchini Sudan Kusini huku matukio ya utekaji nyara, ubakaji na uhaba wa chakula vikishamiri.