Skip to main content

UNMISS yatiwa hofu kuendelea kwa mapigano Mto Nile

UNMISS yatiwa hofu kuendelea kwa mapigano Mto Nile

Kuendelea kwa mapigano katika ukingo wa magharibi mwa Mto Nile kaskazini nchini Sudan Kusini kumefikia kile mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini UNMISS, David Shearer ameelezea kutia hofu.

Taarifa ya UNMISS ikimnukuu msemaji wake inasema kuwa kilichoanza kwa kufyatuliana risasi kati ya kikosi cha serikali cha SPLA na vikosi vya upinzani vya Aguelek kimeyafikia maeneo mengine  hadi kushuhudiwa kwa vikosi vya kijeshi kuwasili  katika eneo hilo.

Mnamo Februari 8, UNMISS ilipokea taarifa za uhasama kati ya SPLA na  vikosi vya upinzani katika maeneo ya Owachi na Tonga, kaunti ya Panyinkang.

Mapigano hayo katika eneo ambalo wengi wa watu ni wa kabila la Shilluk, yamelazimisha wengi kuyakimbia makazi yao. Licha ya wahudumu wa misaada kutumwa katika eneo hilo,  ugawaji wa misaada hautekelezeki, imesema UNMISS.