Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNMISS ahitimisha ziara jimbo la Unity

Mkuu wa UNMISS ahitimisha ziara jimbo la Unity

Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, David Shearer, amehitimisha ziara yake kwenye miji ya Bentiu na Leer iliyoko jimbo la Unity, ambayo ndiyo imeathiriwa zaidi na mzozo unaoendelea nchini humo.

Wakati wa ziara hiyo alitembelea maeneo kadhaa ikiwemo yale yanayoshikiliwa na upande wa upinzani ambako alikutana na wafuasi wa Makamu wa zamani wa Rais Riek Machar.

Wapiganaji hao wamemweleza Bwana Shearer kuwa wanaunga mkono sitisho la mapigano kwenye eneo hilo la Leer wakisema ni hatua inayoweza kusaidia kurejea kwa misaada ya kibindamu na kuchagiza mchakato wa amani.

Akiwa Bentiu alikutana na maafisa wa serikali na wakimbizi wa ndani wanaohifadhiwa katika kituo cha kuhifadhi raia, ikiwa ni kituo chenye idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wa ndani nchini Sudan Kusini.

Pande zote mbili ambazo ni serikali na upinzani kwenye maeneo hayo yamepongeza Umoja wa Mataifa kwa jitihada zake za kufanikisha mawasiliano kati yao.

Bwana Shearer ambaye tayari amerejea Juba, amesema pande hizo zinatambua kuwa mjadala shirikishi wa kitaifa ndio utakaosaidia kusongesha mchakato wa amani.