Skip to main content

Idadi ya wanawake wahandisi bado ni ndogo- UNESCO

Idadi ya wanawake wahandisi bado ni ndogo- UNESCO

Shirika Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO limesema ingawa idadi ya wanawake wanaopata shahada ya uzamili na uzamivu imeongezeka kote duniani, bado idadi ya wanawake wanaosomea uhandisi na sayansi ya kompyuta bado ni ndogo.

Ripoti ya UNESCO kuelekea utekelezaji wa ajenda 2030 inasema ni asilimia 28 tu ya wanawake katika ngazi hizo za shahada husalia watafiti ingawa kuna nchi zilizopiga hatua kama vile Thailand na Ufilipino.

Hata hivyo ripoti hiyo iliyotolewa kuelekea siku ya wanawake na wasichana katika sayansi tarehe 11 mwezi huu, imesema kikanda, katika nchi za Muungano wa Ulaya wanawake watafiti ni asilimia 33 ilhali kwa nchi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara ni asilimia 30, hali inayotia matumaini.

Ripoti inasema baadhi ya nchi idadi imeongezeka kutokana na lengo la wanawake kutaka kukabiliana na ukosefu wa chakula hivyo kusoma uhandisi wa kilimo ilihali kwingineko idadi ni ndogo kutokana na fikra potofu kuwa wanawake hawana uwezo kwenye sayansi.