Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kaya nchini Gambia kupatiwa usaidizi kutoka WFP

Kaya nchini Gambia kupatiwa usaidizi kutoka WFP

Takriban watu 10, 000 nchini Gambia watapatiwa msaada wa fedha kutoka shirika la mpango wa chakula duniani, WFP ili waweze kujinunulia chakula na mahitaji mengine muhimu.

Taarifa ya WFP imesema watu hao ni kutoka kaya zilizokumbwa na kimbunga na mafuriko kwenye ukanda wa pwani, maeneo ya kati na magharibi mwaka 2016.

Watapatiwa jumla ya dola 150 kila kaya kwa kipindi cha miezi mitatu kuhakikisha wana uhakika wa chakula na hivyo kuimarisha hali yao ya lishe.

Mwakilishi wa WFP nchini Gambia, Angela Cespedes amesema wameazimia kusaidia Gambia kukidhi mahitaji ya wananchi ambao mvua za mwaka jana ziliharibu mindombinu ya kijamii, mashamba ya mpunga na mazao mengine.

Bi. Cespedes amesema watashirikiana na wadau wengine kusaidia kukwamua kaya hizo ambazo usajili wao ulifanyika kwa ushirikiano na mamlaka ya taifa ya udhibiti wa majanga, NDMA.