Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Côte d’Ivoire ni tulivu lakini usaidizi bado wahitajika- Mindaoudou

Côte d’Ivoire ni tulivu lakini usaidizi bado wahitajika- Mindaoudou

Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Côte d’Ivoire, Aïchatou Mindaoudou leo amewasilisha ripoti yake mbele Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akisema licha ya nchi hiyo kutikiswa tena wakati wa mchakato wa uchaguzi, wananchi walipiga kura kwa amani na matokeo yakatangazwa katika mazingira ya amani na tulivu.

Amesema kwa ujumla hali ya usalama imeimarika, taarifa za ukiukwaji wa haki za binaadamu zimepungua na mafanikio makubwa ya kisiasa yamepatikana hususan katika upigaji kura ya maoni ya katiba.

Hata hivyo Bi. Mindaoudou ambaye ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNOCI unaomaliza muda wake mwezi Juni mwaka huu, amesema baadhi ya changamoto zitaendelea kuhitaji tahadhari na ushirikiano wa watu na serikali ya Côte d’Ivoire, na kwa msaada wa wadau wao, hususan...

(Sauti ya Mindaoudou)

" Maridhiano ya kitaifa yanayohitaji kusongeshwa mbele na haki ya mpito kuharakishwa; sekta ya usalama inahitaji marekebisho kikamilifu kwa mujibu wa sheria, haja ya kuwaunganisha wapiganaji wa zamani na jamii; kuboresha zaidi haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni nchini Côte d’Ivoire kunahitajika, ikiwa tunataka kuondokana na vitendo vyenye kulemaza viwanda vinavyoaosababishwa na maandamano ya watumishi wa serikali na watu. Kwa pamoja na kwa utengano, vyote vitaleta amani ya muda mrefu nchini Côte d’Ivoire .

Amesema ni dhahiri kuwa UNOCI itaondoka nchini humo katika miezi minne ijayo, na amechukua fursa hiyo kuipongeza serikali ya Côte d’Ivoire na kuwasihi kuendelea na juhudi zao katika mchakato wa amani, kwani hilo tu ndilo litadhihirisha mafanikio halisi ya uwepo wa UNOCI.

Vile vile amezishukuru nchi zilizochangia askari na polisi kwa ajili ya kuisaidia Umoja wa Mataifa katika kuleta amani, na kupongeza ujasiri wa vikosi vya UNOCI huku akitoa rambirambi zake za dhati kwa wanawake na wanaume ambao wamejitoa mhanga katika utumishi wa amani nchini humo.