Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wajumuishwe kwenye jamii ili kuondoa makovu ya vitani-Zerrougui

Watoto wajumuishwe kwenye jamii ili kuondoa makovu ya vitani-Zerrougui

Katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kumefanyika kikao kisicho rasmi cha Baraza Kuu kutathmini miaka 20 tangu kuanzishwa kwa kitengo kinachohusika na ufuatiliaji wa masuala ya ukatili wa watoto vitani.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto katika migogoro ya kivita Leila Zerrougui akizungumza kwenye kikao hicho amesema kuwa matumizi ya watoto vitani huacha makovu makubwa kwenye maisha yao na kwamba ....

(Sauti ya Zerrougui)

“Ili amani iwe endelevu ni lazima tushughulikie pia madhara ya muda mrefu ya vita kwa watoto. Kipaumbele ni watoto waliotumikishwa na vikundi vyenye silaha waachiliwe huru na wajumuishwe kwenye jamii. Mipango ya kuwajumuisha ni muhimu ili kusaidia watoto kukabiliana na kiwewe na kujitambua tena mustakhbali wao na hatimaye kupata stadi zinazohitajika ili wawe watu wenye manufaa kwa jamii zao."

Bi. Zeorougi akasema tangu kuanzishwa kwa ofisi yake mwezi disemba mwaka 1996 zaidi ya watoto 115,000 wameachiliwa na kwamba..

(Sauti ya Zerrougui)

“Kwa miongo miwili iliyopita kwa pamoja tumepata mafanikio makubwa ya kuimarisha ulinzi wa watoto walioathirika kwa mizozo na tukio hili la leo ni dhihirisho juu ya hatua za mafanikio haya na kuangalia mbele jinsi ya kulinda vyema watoto wetu na vizazi vijavyo dhidi ya machungu ya vita.

Miongoni mwa waliohudhuria kikao hicho ni Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Anthony Lake, Ilwad Elman msichana mwanaharakati wa haki za binadamu na mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali juu ya mipango na maendeleo katika kituo cha Elman nchini Somalia na mjumbe maalum wa amani wa Umoja wa Mataifa na mcheza filamu mashuhuri Forest Whitaker.