Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola bilioni 2.1 zasakwa kukwamua Yemen

Dola bilioni 2.1 zasakwa kukwamua Yemen

Umoja wa Mataifa na wadau wa kibinadamu wametangaza ombi la dola bilioni 2.1 kwa ajili ya misaada ya kuokoa maisha kwa watu milioni 12 nchini Yemen kwa mwaka huu wa 2017, ikiwa ni kiwango kikubwa zaidi kuwahi kuombwa kwa ajili ya Yemen.

Akizindua ombi hilo huko Geneva, Uswisi hii leo, mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA Stephen O’Brien amesema usaidizi huo ni muhimu ili kunusuru nchi hiyo inayotumbukia kwenye njaa.

Amesema miaka miwili ya vita imesambaratisha nchi hiyo, watoto, wanawake na wanaume wakihaha kupata misaada, hivyo amesihi jumuiya ya kimataifa kuchangia fedha hizo.

(Sauti ya O’Brien)

“Unaangalia watu milioni 14 ambao hawana chakula, na kati yao miilioni saba au nane hawafahamu mlo wao ujao wanaupata wapi. Na ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, wanawake wanaonyonyesha watoto, wanawake, wazee na wagonjwa ambao wamenasa kwenye hali hii.”

Bwana O’Brien amesema wadau wa kibinadamu wako tayari kusaidia lakini wanachohitaji ni rasilimali za kutosha na kuweza kufika kwa wakati muafaka na bila vikwazo vyovyote pindi mahitaji yanapojitokeza.