Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu kwa maelfu ya watoto Mashariki mwa Ukraine mashakani

Elimu kwa maelfu ya watoto Mashariki mwa Ukraine mashakani

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema maelfu ya watoto mashariki mwa Ukraine wamelazimika kuacha shule, kutokana na mapigano makali yaliyoanza juma lililopita.

UNICEF imesema mapigano hayo mapya yamesababisha watoto 2,600 kutoka shule 13 kwenye eneo linalodhibitiwa na serikali na maelfu wengine kutoka maeneo yasiyo chini ya serikali kukosa masomo.

Takriban shule 5 na mbili za chekechea zimeharibiwa na makombora na kusababisha nyingine 11 kufungwa, hali ambayo UNICEF inasema inazidi kuwa mbaya, ikiathiri zaidi ya watoto 600,000 mashariki mwa Ukraine.

Kutokana na mapigano hayo, UNICEF inasema familia sasa zinaogopa kupeleka watoto wao shuleni kwa hofu ya makombora njiani na mengine ambayo bado hayajalipuka.

UNICEF na wadau wengine wametoa wito kwa pande zote katika mzozo kusitisha ulengaji wa makusudi wa shule, kuheshimu sheria za kimataifa kwa kuhakikisha shule na miundombinu ya raia kamwe hazishambuliwi.

Vile vile wamesihi wadau hao kusitisha mapigano kwa kuzingatia mkataba wa Minsk uliosainiwa mwezi Agosti mwa 2015.