Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ombi la dola milioni 291 latangazwa kukwamua Haiti

Ombi la dola milioni 291 latangazwa kukwamua Haiti

Nchini Haiti, serikali kwa kushirikiana na wadau wa kibinadamu nchini humo ukiwemo Umoja wa Mataifa, wametangaza ombi la dola milioni 291 kwa ajili ya kusaidia wananchi zaidi ya milioni Mbili kwa mwaka huu wa 2017.

Likitajwa kuwa ni mpango wa usaidizi wa kibinadamu kwa mwaka 2017-2018, fedha hizo zinalenga kusaidia wananchi na taasisi za kitaifa kukabili majanga ikiwemo yale ya asili ili hatimaye kuelekea katika njia sahihi ya maendeleo endelevu.

Ombi la sasa limetolewa wakati ambapo ombi la mwaka uliotangulia lilikumbwa na changamoto kadhaa ikiwemo kimbunga Matthew, kipindupindu na ukosefu wa chakula uliochochewa na El nino.

Kwa mantiki hiyo ombi la sasa litachagiza fursa nyingine pia za kukwamua uchumi na kusongesha Haiti.