Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kambi zaidi zahitajika kuhifadhi wakimbizi wa Burundi- UNHCR

Kambi zaidi zahitajika kuhifadhi wakimbizi wa Burundi- UNHCR

Wakati idadi ya wanaokimbia Burundi ikitarajiwa kuvuka nusu milioni hivi karibuni, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, linaomba Tanzania, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC na Rwanda kutoa ardhi zaidi ili kukidhi mahitaji yao ya makaazi. John Kibego na taarifa Kamili.

(Taarifa ya John Kibego)

Kwa mujibu wa William Spindler, msemaji wa UNHCR, idadi ya wakimbizi wa Burundi imeongezeka hasa nchini Rwanda, Tanzania na DRC kufuatia kukwama kwa mazungmuzo ya amani.

Tangu April 2015 idadi ya waliokimbia nchi hiyo ni takribani laki nne.

Kufurika kwa wakimbizi kwenye kambi zilizopo kumeibua changamoto nyingi ikiwemo, utoaji wa huduma za jamii, ulinzi wa watoto na kukwama kwa juhudi za kupinga ukatili wa kijinsia.

(Sauti ya Spindler)

"Hivi sasa Tanzania inahifadhi wakimbizi 222,271, Rwanda 84,866 na DR Congo 32,650. Bila ya ugawaji wa ardhi mpya kupanua uwezo katika kambi zilizopo au kujenga mpya, nchi hizi zitahaha kutoa makazi ya kutosha na huduma zenye kuokoa maisha kwenye kambi hizo."

Kambi ya Lusenda nchini DRC, Mahama nchini Rwanda na Nduta nchini Tanzania ni miongoni mwa kambi zinazohifadhi wakimbizi wengi kupita kiasi.