Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Harakati za kufikisha msaada Syria ni za kusuasua

Harakati za kufikisha msaada Syria ni za kusuasua

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de Mistura ana wasiwasi mkubwa na ugumu wa kufikisha misaada kwa wahitaji 914,000 katika maeneo ya Maday, Zabadani, Foha na Kefraya nchini Syria katika mwezi wa Januari.

Msemaji wa de Mistura, Bi Yara Sharif amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kwamba, kati ya maombi 21 ya msafara wa kupeleka misaada, ni msafara mmoja tu kwa watu 40,000 ndio uliowezekana.

Amesema mwezi Januari ndio uliokithiri ugumu tangu Machi 2016, na kuna umuhimu wa mahitaji ya haraka katika maeneo ambayo hayajapokea msaada wowote kwa zaidi ya siku 100.

(Sauti ya Yara)

"Mjumbe Maalum anatoa wito wa upatikanaji wa msaada usio na masharti na ulio endelevu kwa watu wote milioni 4.72, katika maeneo yaliyo magumu zaidi kufikika nchini kote, ikiwa ni pamoja na zaidi ya watu 600,000 katika maeneo yanayokabiliwa."

Halikadhalika amesema watu milioni 1.8 mjini Aleppo na mashinani wamekatiwa maji, huku chanzo cha maji kikishikiliwa na kundi la kigaidi la ISIS.

Wakati huo huo mazungumzo ya Astana kuhusu kusitishwa kwa mapigano yamekamilishwa jana, na washiriki wa mkutano huo watawasilisha ripoti yao kwa mjumbe huyo mjini Geneva hii leo.