Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yazindua kampeni ya hatari za kukimbilia Yemen

UNHCR yazindua kampeni ya hatari za kukimbilia Yemen

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR leo limezindua kampeni ya kuhamasisha umma juu ya hatari wanazoweza kukumbana nazo watu wanaovuka ghuba ya Aden na bahari ya Sham kutoka Afrika kuelekea Yemen ambayo imegubikwa na vita.

Kampeni hiyo kupitia mwanamuziki nyota na mkimbizi wa zamani Maryam Mursal inatumia wimbo wenye ujumbe maalum wa kutaka watu kufikiria kwa kina kabla ya kuamua kuingia Yemen.

Mkurugenzi wa UNHCR kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini Amin Awad amesema wana jukumu la kupaza sauti na kuelimisha hatari hizo kwani idadi kubwa ya wahamiaji hawana taarifa sahihi za hali halisi nchini Yemen.

Zaidi ya wakimbizi na wahamiaji 117,000 waliingia Yemen mwaka 2016 ambapo UNHCR imesema wengi walilaghaiwa na kufanya safari za boti baharini, safari zilizo na machungu kwa ahadi za kupata maisha bora.

Yemen imekuwa vitani tangu mwezi Machi mwaka 2015 ambapo watu zaidi ya 7,000 wameuawa, huku 44, 000 wakijeruhiwa na zaidi ya milioni mbili hawana makazi.