Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICC ni muhimu kwa Afrika, majadiliano yafanyike kubaini udhaifu-Dieng

ICC ni muhimu kwa Afrika, majadiliano yafanyike kubaini udhaifu-Dieng

Mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu  kuzuia mauaji ya kimbari Adama Dieng  amesema ingawa ilikuwa ni mafanikio makubwa kuanzisha mkataba wa Roma wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC, bado chombo hicho kinapaswa kuwa tayari kusikiliza hofu za wale ambao kinawahudumia.

Bwana Dieng amesema hayo katika maoni yake yaliyochapishwa kwenye gazeti la The East African wakati huu ambapo tayari nchi tatu za Afrika zimetangaza kujitoa ilhali nyingine zikipanga kufanya hivyo.

Ametaja vyombo husika kuwa ni ofisi ya rais wa ICC, mwendesha mashtaka na msajili akisema mashauriano kuhusu mustakhbali yahusishe.

(Sauti  Adama Dieng)

“Wanachama, wasio wanachama,  mashirika yasiyo ya kiserikali, asasi za kiraia, na waathirika  kwasababu hakuna anayependa kuona siku moja kesi yake ikipuuzwa."

Amesema wakati huu ambapo mizozo inaendelea Syria, Yemen, Iraq, Sudan Kusini na kwingineko, si wakati sahihi kuachana na mahakama hiyo na badala yake pande husika ziazimie kuiimarisha ili kuwajibisha watekelezaji wa uhalifu huo.

( Sauti Adama Dieng)

“Kama umeshawahi kuwa muathirika wa uhalifu mkubwa na unaona nchi yako haichukui hatua yoyote, basi utapata ahueni kutoka ICC. Na kile muhimu leo ni kuhakikisha ICC inaendelea kufanya kazi- ICC ibakie, ndio  naweza kusema, chombo cha haki, kikitoa haki kwa wale wanaohitaji.”