Skip to main content

Idadi ya waliouawa Afghanistan 2016 yavunja rekodi- UNAMA

Idadi ya waliouawa Afghanistan 2016 yavunja rekodi- UNAMA

Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa pande zote zinazopingana nchini Afghanistan kuchukua hatua za haraka ili kusitisha mapigano ambayo yanasababisha vifo vya raia na wengine kubakia na ulemavu.

Wito huo huo umetolewa na mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA, Tadamichi Yamamoto kufuatia kutolewa kwa ripoti inayoonyesha kuwa zaidi ya watu 3400 waliuawa mwaka jana huku wengine 7920 wakijeruhiwa.

Kiwango hicho ni cha juu zaidi cha vifo tangu kuanza kuwekwa kwa kumbukumbu hizo mwaka 2009.

Bwana Yamamoto ambaye pia ni mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan amesema kuua na kuachia watu vilema kunaweza kuwa uhalifu wa kivita hivyo ametaka pande hizo kuangalia upya utekelezaji wa operesheni zao.

Naye kamishna mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad al Hussein ametaka pande zote kupunguza matumizi ya silaha za kulipuka kwenye makazi ya watu.