Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM walaani marufuku dhidi ya asasi za kiraia Burundi

UM walaani marufuku dhidi ya asasi za kiraia Burundi

Kundi la wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa leo wamelaani marufuku na kusimamishwa kwa muda kwa asasi za kiraia, iliyotolewa hivi karibuni na serikali ya Burundi.

Kundi hilo limeonya kile lilichokiita madhara ya vipingamizi ,vizuizi na unyanyapaa utokanao na sheria dhidi ya asasi za kiraia katika muktadha wa kukandamiza watetezi wa haki za binadamu.

Taarifa ya wataalmu hao inafuatia marufuku dhidi ya asasi tano za kiraia iliyotolewa Oktoba 19 mwaka jana, na kufuatiwa na na marufuku dhidi ya ITEKA ambayo ni miongoni mwa asasi za kiraia za haki za binadamu inayoongoza Burundi, huku pia asasi nyingine iitwayo OLUFAD inayotetea utawala bora na kupinga rushwa ikipigwa marufuku.

Kwa mujibu wa talaamu hao wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, bunge la nchi hiyo lilipitisha sheria baada ya marufuku hizo, sheria zilizolenga kuzidhibiti asasi za kiraia za kitaifa na kimataifa ikizitaka kupata idhini ya kazi zao kwa waziri wa mambo ya ndani pamoja na kuhamisha fedha kutoka nje kupitia benki kuu.

Wamesema kuwa hatua hizo ambazo ni mfululuzo wa kuzorota kwa haki za binadamu nchini Burundi, zinaendeleza madhila kwa watetezi wa haki hizo na kuongeza kuwa wale ambao hawajaondoka nchini humo wanahofia maisha yao huku wakitishiwa kuwekwa kizuizini, kuteswa na kutoweka.