Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP, Ubelgiji kutumia ndege zisizo na rubani katika dharura za kibinadamu

WFP, Ubelgiji kutumia ndege zisizo na rubani katika dharura za kibinadamu

Shirika la mpango wa chakula duniani WFP na serikali ya Ubelgiji wanafanya uzinduzi wa mpango wa kuchunguza matumizi ya ndege zisizo na rubani (UAVs au drones) katika usaidizi wa dharura wa kibinadamu.

Kwa mujibu wa taarifa ya WFP, warsha ya kwanza ya kimataifa juu ya uratibu wa kibinadamu wa UAV imeanza leo mjini Brussels kuleta pamoja wataalam kutoka sekta za kibinadamu, kielimu, serikali na sekta binafsi.

Utumiaji wa ndege hizo unazidi kutambuliwa na mashirika ya kibinadamu kwa ufanisi na uwezo katika kukabiliana na maafa imesema taarifa hiyo.ambapo teknolojia hiyo inaweza kusaidia mashirika ya kibinadamu kwa haraka kukusanya taarifa, kufikisha takwimu kwa usahihi na kutoa mifumo ya ufuatiliaji salama kwenye shughuli za dharura.

Mkurugenzi Mtendaji wa WFP Ertharin Cousin ameishukuru serikali ya Ubelgiji kwa mchango wao wa Euro 500.000, akiongeza kuwa katika kipindi cha chini ya muongo mmoja, gharama ya kukabiliana na maafa ya kibinadamu duniani kote imeongezeka kutoka €uro bilioni 3 kwa zaidi ya €uro bilioni 20.