Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili wa kutisha dhidi ya Rohingya umetekelezwa Myanmar: UM

Ukatili wa kutisha dhidi ya Rohingya umetekelezwa Myanmar: UM

Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa Ijumaa imeeleza kuwa ukatili wa kutisha dhidi ya watu wa Rohingya, ikiwa ni pamoja na ubakaji unaofanywa na magenge ya watu, mauaji yakijumuisha watoto na vijana wadogo, kupigwa, kutoweka na ukiukwaji mwingine mkubwa wa haki za binadamu umetekelezwa na vikosi vya usalama vya serikali ya Myanmar katika eneo la Kaskazini la Maungdaw jimbo la Rakhine nchini Myanmar.

Kwa mujibu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ripoti hiyo imetokana na mahojiano walioyofanyiwa waathirika walioko upande wa pili wa mpaka nchini Bangladesh. Ravina Shanmdasani ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu

(SAUTI YA RAVINA)

“kati ya watu 204 waliohojiwa na timu ya uchughuzi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu wengi wao wameripoti kushuhudia mauaji na karibu nusu jamaa wa familia zao wameuawa na wengine kutoweka. Kati ya anawake 101 waliohojiwa Zaidi ya nusu wameripoti kubakwa au kufanyiwa ukatili mwingine wa kingono”

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid R’aad Al Hussein amesema ukatili dhidi ya jamii ya Rohingya wakiwemo watoto hauvumiliki , na kuhoji ni binadamu wa aina gani anamchoma kisu mtoto na kumuua akililia maziwa ya mama yake.

Amesema jeshi linalostahili kulinda watu ndio linalowaadhibu na kuongeza kuwa ukatili huo umefurutu ada.